Deuteronomy 13

Kuabudu Miungu Mingine

1 aKama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2 bikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” 3 ckamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. 4 dNi Bwana Mwenyezi Mungu wenu ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. 5 eHuyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

6 fKama ndugu yako hasa, au mwanao au binti yako, au mke umpendaye, au rafiki yako wa karibu sana akikushawishi kwa siri, akisema, “Na twende tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo ninyi wala baba zenu hamkuifahamu, 7miungu ya watu wanaowazunguka, ikiwa karibu au mbali, kutoka mwisho mmoja wa nchi mpaka mwingine), 8 gusikubali wala usimsikilize. Usimhurumie! Usimwache wala usimkinge. 9 hHakika ni lazima auawe. Ni lazima mkono wako uwe wa kwanza katika kumuua kisha mikono ya watu wengine wote. 10 iMpigeni kwa mawe mpaka afe, kwa sababu alijaribu kuwageuza mtoke kwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu ambaye aliwatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. 11 jKisha Israeli wote watasikia na kuogopa, wala hakuna mmoja miongoni mwenu atakayefanya uovu tena.

12 kKama mkisikia ikisemwa kwamba moja ya miji ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawapa mkae ndani yake 13 lkuna wanaume waovu wameinuka miongoni mwenu na wamewapotosha watu wa mji, wakisema, “Twendeni tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo hamkuifahamu), 14 mndipo itakubidi kuuliza, kupima na kuchunguza kwa makini. Kama ni kweli, tena ikihakikishwa kwamba jambo hili lichukizalo limefanyika miongoni mwenu, 15 nkwa hakika ni lazima mwaue kwa upanga wale wote wanaoishi katika mji ule. Uharibuni kabisa, pamoja na watu wake na mifugo yake. 16 oKusanyeni nyara zote za mji katika uwanja wa wazi na kuuchoma mji kabisa pamoja na nyara zake zote kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu. Utabaki kuwa magofu milele na hautajengwa tena. 17 pHakuna kimoja kati ya vitu vilivyolaaniwa kitakachokutwa mikononi mwenu, ili Bwana ageuze hasira yake kali. Atawahurumia na kuwa na rehema kwenu pia kuongeza idadi yenu, kama alivyowaahidi baba zenu, 18 qkwa sababu mnamtii Bwana Mwenyezi Mungu wenu, mkizishika amri zake zote zile ninazowapa leo na kufanya lile lililo jema machoni pake.
Copyright information for SwhKC